
Rubani wa ndege anayedaiwa kumdhalilisha afisa wa polisi wa kike nchini Kenya amefutwa kazi.
Rubani
huyo, ambaye ni raia wa Uingereza, alikuwa na ndege aina ya helikopta
nambari 5Y-DSN iliyokuwa imembeba Naibu Rais William Ruto wakati wa
ziara yake mji wa Ndunyu Njeru, jimbo la Nyandarua katikati mwa nchi
hiyo Jumapili.
Kampuni ya Kwae Island Development (KIDL) ambayo humiliki helikopta hiyo imesema kisa hicho ni cha kusikitisha.
“KIDL
imefahamu kutoka kwa mitandao ya kijamii na vyanzo vingine vya habari
kwamba Alistair Llewelyn alihusika katika kisa tarehe 20 februari 2016.
KIDL inasikitishwa sana na kisa hiki na inajitenga kabisa na vitendo vya
Alistair Llewelyn,” taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Marco
Brighetti, mmiliki wa kampuni hiyo inasema.
“KIDL inaheshimu maafisa wapolisi wa kiume na kike wa Kenya na inalaani kabisa vitendo vya Alistair Llewelyn.”
Bw
Llewelyn amejisalimisha kwa polisi katika kituo cha Kilimani. Msemaji wa
polisi George Kinoti amesema mshukiwa huyo anatarajiwa kufikishwa
kortini Jumatano.
Video iliyochukuliwa na mmoja wa walioshuhudia
kisa hicho cha Jumapili imesambaa sana mtandaoni watu wakitaka hatua
zichukuliwe dhidi ya rubani huyo.

Afisa wa mawasiliano wa Bw Ruto, Bw David Mugonyi, amesema kiongozi huyo amefahamishwa kuhusu kisa hicho.
“Naibu Rais amewaagiza polisi kuchukua hatua mara moja. Naibu Rais anaheshimu polisi wetu wenye bidii ambao hufanya kazi saa nyingi kulinda nchi. Kisa hiki hakikubaliki, na ni cha kusikitisha na nimewataka polisi kuchunguza kitendo hicho cha rubani huyo,” taarifa yake imesema.
Reviews:
Post a Comment