![]() |
Bw Kukan amesema ni dhahiri Tume ya Uchaguzi haikujifunza kutoka kwa uchaguzi wa 2011 |
Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya wamekosoa jinsi uchaguzi mkuu wa Uganda uliendeshwa na kusema mabadiliko makubwa yanahitajika.
Wakihutubia wanahabari, viongozi wa ujumbe kutoka Muungano wa Ulaya wamesema kulitokea kasoro nyingi.
Mwangalizi
mkuu wa Umoja wa Ulaya Eduard Kukan amewaambia wanahabari kwamba ni
dhahiri Tume ya Uchaguzi ya Uganda haikujifunza kutokana na mapendekezo
yaliyotolewa baada ya uchaguzi mkuu wa 2011.
Aidha, amesema
haikuwa haki kufunga usajili wa wapiga kura Mei mwaka jana akisema hatua
hiyo iliwafungia watu waliotimiza umri wa miaka 18 baada ya tarehe
hiyo.
"Tume haina uwazi na wadau hawana imani nayo. Tume haina
uwazi katika kufanya maamuzi na katika kuwafahamisha wapiga kura kwa
wakati na kwa ufasaha,” amesema.
Bw Kukan amesema kucheleweshwa
kwa karatasi na vifaa vya kupigia kura pamoja na kuchelewa kuanza kwa
upigaji kura siku ya uchaguzi kuliathiri imani ya watu katika zoezi
hilo.
Ameshutumu pia kukamatwa na kuzuiliwa kwa kiongozi wa upinzani Dkt Kizza Besigye pamoja na kufungwa kwa mitandao ya kijamii.
Mwangalizi
mkuu wa Bunge la Ulaya Jo Leinen kwa upande wake amesema wagombea wote
hawakupewa nafasi sawa katika vyombo vya habari na wanasiasa pamoja na
raia waliounga mkono upinzani walihangaishwa.
Amesema pia kwamba fedha za serikali na chama lazima kutenganishwa.
"Kuna mengi sana ambayo yanafaa kurekebishwa,” amesema.
![]() |
Dkt Besigye amekamatwa na polisi mara tatu wiki hii |
Ameshutumu kukamatwa na kuzuiliwa kwa Dkt Besigye akisema hatua hiyo iliongeza tu wasiwasi.
Matokeo kamili ya uchaguzi wa urais yanatarajiwa kutangazwa kabla ya saa kumi alasiri leo.
Matokeo yaliyotangazwa kufikia sasa yanaonyesha Rais Yoweri Museveni anaongoza akiwa na zaidi ya asilimia 60 ya kura dhidi ya Dkt Kizza Besigye aliye na asilimia 34 ya kura zilizohesabiwa.
Reviews:
Post a Comment