Ted Cruz amshinda Trump mchujo wa Iowa

Seneta wa Texas Ted Cruz ameshinda mchujo wa uchaguzi wa mgombea wa uchaguzi wa Republican katika jimbo la Iowa, Marekani.

Huo ndio mchujo wa kwanza katika uchaguzi wa urais wa 2016 ambao utafanyika baadaye mwezi Novemba.
Cruz amepata asilimia 28 ya kura.
"Huu ni ushindi wa wahafidhina jasiri," mgombea huyo amesema baada ya kubainika kwa ushindi wake.
Mfanyabiashara Donald Trump alikuwa akiongoza kwenye kura za maoni kabla ya kura kupigwa lakini sasa amekuwa wa pili na asilimia 24.
Seneta wa Florida Marco Rubio amefanya vyema kuliko ilivyotarajiwa, na akamaliza nambari tatu na asilimia 23.
Kura za mchujo wa chama cha Democratic bado zinahesabiwa.

Matokeo ya Iowa

Chama cha Republican, 99% ya kura:

  • Ted Cruz: 28%, wajumbe wanane
  • Donald Trump: 24%, wajumbe saba
  • Marco Rubio: 23%, wajumbe saba
  • Ben Carson: 9%, wajumbe watatu

Chama cha Democratic, 99% ya kura:

  • Hillary Clinton: 50%, wajumbe 22
  • Bernie Sanders 50%, wajumbe 21
Asilimia 85 ya kura ambazo zimehesabiwa zinaonyesha pengo kati ya Hillary Clinton na mshoshialisti wa chama cha Democratic Bernie Sanders ni 1% pekee.
Akizungumza baada ya matokeo kujulikana, Marco Rubio amempongeza Bw Cruz na kusema ndiye mgombea ambaye anaweza kuunganisha chama cha Republican ambacho kimegawanyika.

Dakika chache baadaye, Bw Trump alipanda jukwaani katika ukumbi mwingine na kumpongeza seneta huyo wa Texas, na kusema anaridhika kumaliza katika nambari mbili.
Wagombea wawili wamejiondoa kinyang’anyironi.
Duru za karibu na mgombea wa Democratic Martin O'Malley, aliyekuwa gavana Maryland, zimeambia BBC kwamba atasitisha kampeni yake, na kufanya ushindani mkali sasa kuwa kati ya wagombea wawili.
Upande wa Republican, gavana wa zamani wa Arkansas Mike Huckabee ameandika kwenye Twitter kwamba atasitisha kampeni yake.

Reviews:

Post a Comment

PRINCE PRODUCT © 2014 - Designed by Templateism.com, Plugins By MyBloggerLab.com | Published By Gooyaabi Templates

Contact us

Powered by Blogger.