Ushirikiano wa Zitto, Mbowe waacha maswali
Kuna siri gani? Ushirikiano wa mahasimu wa kisiasa wa upinzani; Zitto Kabwe wa ACT Wazalendo (Kigoma Mjini) kwa upande mmoja na Freeman Mbowe wa Chadema (Hai) na Ukawa kwa upande mwingine kupinga uamuzi wa Serikali bungeni umevuta hisia za Watanzania na kuacha maswali iwapo ni urafiki wa mashaka au ni wa muda mfupi.

Uhusiano huo wa Zitto na viongozi mbalimbali wa Ukawa ambao umedumu kwa wiki moja sasa, umeibua maswali kama utadumu au ni kwa ajili ya kusimamia hoja zao bungeni.
 Zitto na Mbowe walionekana wakitabasamu pamoja Jumanne iliyopita baada ya kukutana kutoa tamko juu ya tangazo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuzuia kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia TBC1 kwa madai ya kubana matumizi ya Serikali.

Tangu Zitto afukuzwe Chadema na kujiunga na ACT- Wazalendo Machi 21, mwaka 2015 kabla ya kuanza kutengwa na viongozi hao wa Ukawa kwa siku za karibuni ameonekana kuwa karibu na umoja huo wa katiba ya wananchi.

Kwa mara ya mwisho, viongozi hao waliunganisha uhusiano wao katika sakata la Escrow mwaka jana lakini baada ya hapo waliendelea kushambuliana hususani wakati wa kampeni za uchaguzi hatua iliyowachanganya zaidi wafuasi wa mabadiliko wa vyama vya upinzani.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, huenda Zitto amebaini kuwa akiendelea kuwa mpinzani pekee asiyekuwa ndani ya Ukawa na asiyekuwa CCM, atakuwa mpweke kisiasa na huenda akaishia kule walikoishia Augustino Mrema aliyekuwa mbunge wa Vunjo na John Cheyo (Bariadi Mashariki) waliokaa bungeni bila kushirikiana na wapinzani wenzao na sasa wameanguka.

Zitto na baadhi ya viongozi wa Chadema na Ukawa wamekuwa wakivutana mitaani na mitandaoni kwa kauli za maudhi tangu Machi 9, mwaka jana, Chadema ilipotangaza kumvua rasmi uanachama kwa madai ya kuendesha mipango ya usaliti wa chama.

Aprili mwaka jana, akiwa wilayani Kyerwa, Mbowe alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akisema hawatamruhusu Zitto kujiunga na Ukawa.

Mbowe alitoa kauli hiyo akijibu ombi la ACT la Aprili 15, 2015 kupitia Zitto kwamba, chama hicho kilikuwa tayari kujiunga na Ukawa kama walivyotaka baadhi ya viongozi wa umoja huo akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Katika ufafanuzi wake, Mbowe alisema hawamwamini tena Zitto kwa madai kuwa akiingia Ukawa atakuwa akivujisha siri za umoja huo kwenda CCM lakini Zitto alisema Taifa limekuwa na shauku ya ACT kushirikiana na vyama vingine kama njia ya kufanikisha malengo ya kuitoa CCM madarakani.

Vilevile Aprili mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, alisema Chadema haiko tayari kuikaribisha ACT-Wazalendo ndani ya Ukawa kutokana na kile alichosema ‘ni adui kwao’.

Tofauti na hali hiyo, tangu mkutano wa pili wa Bunge kuanza, wanasiasa hao wameonekana kushirikiana katika kujenga hoja dhidi ya zile za wabunge wenzao wa CCM au Serikali.Maoni ya wachambuzi

Akizungumzia uhusiano huo, Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) alisema katika kanuni ya siasa duniani kote hakuna uadui wala urafiki wa kudumu miongoni mwa wanasiasa.

Alifafanua kuwa uhusiano wa kisiasa unatabiriwa na hali ya kisiasa kwa wakati husika.

“Kinachoendesha mahusiano ya wanasiasa ni masilahi yanayojitokeza kwa wakati huo. Zitto au Ukawa hawezi kukwepa kuunga mkono hoja zenye masilahi kisiasa kwa upande wao, mfano waliwahi kuungana tena kwenye Escrow lakini baada ya hapo kila mmoja aliendelea na mipango yake,” alisema Profesa Bakari.

Mchambuzi huyo alisema uhusiano wa wanasiasa hao unaweza kuimarika bila hata kuungana ndani ya Ukawa. Alisema kinachotazamwa si uhusiano mzuri wakati wote bali ni mambo gani yanayoweza kuwafanya kuwa pamoja.

“Mnaweza kutoaminiana kabisa lakini mkajikuta mnashirikiana pamoja, ni jambo la kawaida na Watanzania wanatakiwa kulitambua hilo, Ukawa wanaweza kuwa wanamhitaji Zitto na yeye mwenyewe hawezi kusimama pekee bila Ukawa.”

Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema pamoja na tofauti za wanasiasa hao, hatashangaa Zitto kuingia Ukawa lakini atasikitishwa endapo Ukawa itamkataa alisema Zitto ni mwanasiasa tegemeo na anayeweza kuleta mabadiliko ndani ya chama chochote.

“Uadui unapokuwa umefanyika unaweza kuwa na ukweli au kutokuwa na ukweli lakini kwa bahati mbaya wafuasi ndiyo wanabakia kwenye uadui wa kudumu,” alisema.

Reviews:

Post a Comment

PRINCE PRODUCT © 2014 - Designed by Templateism.com, Plugins By MyBloggerLab.com | Published By Gooyaabi Templates

Contact us

Powered by Blogger.