 |
Vitunguu swaumu (Garlics)
|
Kitunguu swaumu ni jamii ya vitunguu ambayo kwa kitaalamu huitwa Allium sativum.
Jamii hii ilianza kutumika katika mabara mbalimbali duniani hususani
Asia, Afrika na Ulaya takribani miaka 6000 iliyopita. Matumizi makuu
nyakati hizo yakiwa viungo katika mboga na tiba.
Kitunguu
swaumu kimetajwa kwenye vitabu mbalimbali vya dini vikielezea faida
zake katika kutibu maradhi mbalimbali yasababishwayo na bakteria,
matatizo katika mapafu, matatizo katika mfumo wa umen'genyaji chakula,
na matatizo ya kuishiwa nguvu.
Historia inaonesha kuwa,
vitunguu swaumu vilianza kutumika China mwaka 510 K.K na pia vilitumiwa
na wanajeshi wa Ugiriki na Roma. Aidha wasafiri wa vyombo vya baharini
na vijijini pamoja na wakulima barani Afrika walivitumia sana.
Mwaka 1858, mtafiti na mwanasayansi wa nyakati hizo, Louis
Pasteur aligundua uwezo wa kitunguu swaumu katika kuua vimelea
mbalimbali vinavyosababisha magonjwa, na hivyo vikaanza kutumika kama
dawa ya kusafishia vidonda na kuzuia kidonda ndugu hasa zama za vita ya
kwanza na pili ya dunia. Isitoshe, mpaka sasa zipo dawa kadhaa
zilizotengenewa kwa kutumia jamii hii ya vitunguu swaumu ikiwemo dawa
ya kusafisha mdomo (mouth wash) ingawa watumaiji wake wengi
huilalamikia dawa hiyo kwa sababu ya harufu mbaya ya dawa hiyo
inayowasababishia kunuka kwa mdomo.
Faida za vitunguu swaumu
Katika
tafiti mbalimbali vitunguu swaumu vimeonekana kuwa na uwezo wa kutibu
maambukizi ya bakteria, fangasi na virusi vya aina mbalimbali. Aidha
husaidia kuzuia magonjwa ya moyo ikiwemo kuondoa lijamu katika mishipa
ya damu na hivyo kusaidia katika kurekebisha shinikizo la damu. Faida
nyingine za vitunguu swaumu ni pamoja na
Kutibu saratani ikiwemo saratani ya tumbo na utumbo
mkubwa. Tafiti zinaonesha idadi ndogo ya wagonjwa wa saratani katika
nchi ambazo wakazi wake wana utamaduni wa kutumia vitunguu swaumu kwa
wingi.
Vitunguu swaumu husaidia kudhibiti kiwango
cha sukari katika damu. Hata hivyo inashauriwa kwamba wagonjwa wa
kisukari wanaotumia sindano za insulin wasitumie kitunguu swaumu kwa
wingi mpaka watakaposhauriwa na daktari.
Huzuia kusanyiko la chembe sahani zinazosaidia kuganda kwa damu (platelet aggregation)
Husaidia ufyozwaji wa thiamin, hivyo kusaidia kuepusha mwili na ugonjwa wa beriberi
Ina kiasi kikubwa cha vitamini C ambayo husaidia kuzuia ugonjwa wa kiseyeye
Hutumika kutibu magonjwa nyemelezi kama toxoplasmosis, hasa kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.
Ushahidi wa Kitafiti
Katika
utafiti uliofanyika nchini Czech ilionekana kuwa matumizi ya vitunguu
swaumu yalisaidia sana katika kupunguza kusanyiko la lijamu
(cholesterol) pamoja na mafuta yasiyofaa mwilini (low density
lipoproteins) katika mishipa ya damu. Aidha, mwaka 2007 BBC iliripoti
matumizi ya vitunguu swaumu katika kusaidia kumkinga mtumiaji dhidi ya
aina fulani ya mafua iliyosababishwa na virusi. Mwaka 2010, ulifanyika
utafiti mwingine ambao ulijumuisha wagonjwa 50 wenye shinikizo la damu
sugu ambalo lilikuwa ni vigumu kudhibitiwa hata kwa matibabu
yaliyozoeleka ya dawa na njia nyingine. Kama njia ya kuchunguza ufanisi
wa vitunguu swaumu katika kutibu shinikizo la damu, baadhi ya wagonjwa
hao walipewa vitunguu swaumu wakati wengine walipewa dawa isiyohusika
na matibabu ya shinikizo la damu (au placebo). Ilionekana kuwa wale
waliopewa vitunguu swaumu kama dawa ya shinikizo la damu walionesha
maendeleo mazuri kwa vitunguu swaumu kuweza kushusha vizuri kiwango cha
shinikizo la damu, hususani systolic pressure, tofauti na wale
waliopewa placebo.
Nini siri ya kitunguu swaumu?
Sifa kuu zinazokifanya kitunguu swaumu kuwa na uwezo na faida
zilizoainishwa hapo juu ni kule kuwa kwake na viasili kadhaa
(ingredients) ambavyo vinafanya kazi tofauti tofauti. Uwezo wake wa
kiutendaji unatokana na mambo yafuatayo;
Vina uwezo wa kusababisha kutanuka kwa mishipa ya damu (vasodilation)
kwa kubadilisha polysulfides zilizopo ndani yake kuwa hydrogen sulfides
kwenye seli nyekundu za damu.
Husaidia uthibiti
wa kiwango cha sukari mwilini kwa kushusha kiwango cha kemikali ya
homocystine na kupunguza madhara ya kisukari.
Iwapo
vitapondwa pondwa vizuri, vitunguu swaumu hutoa kemikali iitwayo
Allicin ambayo ni dawa dhidi ya bateria, na phytoncide ambayo huua
fangasi wa aina mbalimbali.
Harufu mbaya ya kitunguuu swaumu hutokana na gesi aina ya hydrogen sulfide ambayo inayotolewa baada ya kuvila.
Nini Madhara ya vitunguu swaumu?
Ukiacha faida zake, vitunguu swaumu pia vina hasara na madhara mbalimbali kwa mtumiaji. Madhara hayo ni pamoja na;
Harufu mbaya mdomoni ambayo hutokana na kemikali ya AMS (allyl
methyl sulfide). Harufu mbaya hii, hata hivyo, yaweza kupunguzwa kwa
kunywa maziwa au kunywa maji mengi.
Kwa baadhi ya watumiaji, vinaweza kuwaletea mzio au mcharuko mwili (allergies au inflammatory reactions)
Kichefuchefu, Kutapika na kuharisha.
Huweza kusababisha hatari ya kuvuja damu, kwa sababu huzuia kazi ya
seli sahani (platelets) zenye kusaidia kuganda kwa damu kushindwa
kufanya kazi yake vizuri, na hususani kwa mama wajawazito, baada ya
upasuaji au mara baada ya kujifungua.
Huingiliana
katika utendaji kazi wake na dawa kadhaa kama vile warfarin,
antiplatelets, saquinavir, dawa za shinikizo la damu kwa ujumla hasa
calcium channel blockers, na antibiotiki za jamii ya quinolone kama vile
ciproflaxacillin.
Aidha, vinaelezwa pia kuwa na madhara kwa wanyama jamii ya paka na mbwa.
Reviews:
Post a Comment