
Washukiwa zaidi wamekamatwa na
maafisa wa polisi nchini India kuhusiana na kisa ambapo mwanafunzi
Mtanzania alipigwa na kuvuliwa nguo mjini Bangalore.
Washukiwa wengine wanne wamekamatwa na kufikisha tisa, jumla ya washukiwa wanaozuiliwa na polisi.
Maafisa watatu wa polisi pia wamesimamishwa kazi, wakisubiri kufanyiwa uchunguzi.
Watatu
hao wanatuhumiwa kukataa kupokea malalamiko kuhusu kushambuliwa kwa
mwanafunzi huyo wa kike wa umri wa miaka 21 pamoja na wenzake wa tatu.
Balozi wa Tanzania nchini India John WH Kijazi anatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya ndani ya jimbo la Karnataka.
Baadaye, atakutana na wanafunzi waliodhalilishwa karibu na chuo chao.
Maafisa wawili kutoka afisi ya wizara ya mambo ya nje ya India wataandamana na balozi huyo.
Kisa
cha kushambuliwa kwa wanafunzi hao kimeshutumiwa vikali na serikali ya
Tanzania ambayo imeitaka India kuhakikisha usalama wa wanafunzi
wanaoishi na kusomea humo.
Watanzania mtandaoni pia wamekuwa wakishutumu kisa hicho na kuitaka serikali kuchukua hatua.
Tangu kutokea kwa kisa hicho, wanafunzi wengi kutoka Tanzania wamekuwa wakihofia usalama wao.
Reviews:
Post a Comment