
![]() |
Jaji Tunoi amekanusha madai yaliyotolewa dhidi yake |
Jaji mmoja wa Mahakama ya Juu
nchini Kenya Phillip Tunoi amepatikana na hatia ya kukiuka maadili ya
kazi baada ya uchunguzi uliofanywa na kamati iliyoundwa na Tume ya
Huduma za Mahakama.
Jaji Tunoi amepatikana na hatia ya
"kujihusisha kwa njia isiyofaa" na mtu ambaye alikuwa akimwakilisha
mhusika katika kesi ya uchaguzi, jambo amablo ni ukiukaji wa maadili.
Jaji Mkuu Willy Mutunga amempendekezea Rais Uhuru Kenyatta aunde jopo maalum kwa mujibu wa Katiba.
Jopo hilo litakuwa na jukumu la kuchunguza kikamilifu madai yaliyotolewa dhidi ya Jaji Tonui.
Kwa mujibu wa katiba, Jaji wa Mahakama ya Juu anaweza tu kuondolewa kazini baada ya kuchunguzwa na jopo.
Ripoti ya kamati hiyo
iliyofanya uchunguzi kwa kipindi cha wiki moja inasema madai ya ulaji rushwa dhidi ya jaji huyo hayajaweza kuthibitishwa, na hilo sasa limeachiwa jopo kuchunguza.
Jaji
huyo anatuhumiwa kupokea hongo ya $2 milioni ili apendelee upande mmoja
kwenye kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans
Kidero.
Dkt Kidero na Jaji Tunoi wote wawili wamekanusha madai hayo.
Iwapo
atapatikana na hatia na kuondolewa afisini, atakuwa jaji wa pili wa
Mahakama ya Juu kuondoka afisini kwa madai ya kukiuka maadili.
Naibu
Jaji Mkuu wa zamani Nancy Baraza alijiuzulu Januari 2012, baada ya jopo
kuundwa kuchunguza madai kwamba alimnyanyasa mlinzi wa kike katika
jumba moja la biashara jijini Nairobi.
Reviews:
Post a Comment